Monday, 9 January 2017

Simba yaibamiza Jang'ombe Boys 2-0

Baada ya dakika 90 za Mwamuzi Simba imetoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 na kusonga hatua ya nusu fainali ya michuano hii ambapo Katika mchezo wa leo, mabao yote ya Simba SC yamefungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo moja kila kipindi.

Mavugo aliyesajiliwa Simba SC msimu huu kutoka Vital’O ya kwao Burundi, alifunga bao la kwanza dakika ya 11  kwa shuti baada ya kuukuta mpira uliorudi baada ya kuogonga nguzo ya lango kufuatia shuti la winga Shiza Kichuya aliyepokea pasi nzuri ya mshambuliaji mzawa Juma Luizio

Mavugo akafunga bao la pili dakika ya 53 kwa shuti kali tena baada ya kupokea pasi ya Kichuya pembeni kulia na kumkokota beki wa Jang’ombe hadi kwenye 18 kabla ya kufunga.

Bao hilo likawafanya Jang’ombe Boys wapoteane na kuwapa fursa Simba SC walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kutawala zaidi mchezo.

Kilichofuatia ni kasi ya mashmbulizi mfululizo langoni mwa Jang’ombe Boys na kosa kosa za mabao ya wazi hadi filimbi ya mwisho. Baada ya mchezo huo, Mavugo akachaguliwa kuwa mchezaji bora.

Nahodha Jonas Mkude akasema wamefurahi kwa ushindi huo na kuongoza Kundi A na kwamba kuelekea mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya mahasimu, Yanga hawana wasiwasi.

“Sisi tumejiandaa vizuri, ni matumaini yetu na wao wamejiandaa vizuri, mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi, baada ya maandalizi tutakutana tutacheza, utakuwa mchezo mzuri, kipimo kizuri kwetu na kwao, dakika 90 zitaamua,”.

Kikosi cha Simba kilikuwa; Peter Manyika, Janvier Besala Bokongu/Vincent Costa dk78, Mohammed Hussein ‘Thabalala’,  Anbdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Hijja Ugando dk71, Muzamil Yassin/James Kotei dk46, Pastory Athanas, Laudit Mavugo/Jamal Mnayte dk55 na Juma Luizio/Moses Kitundu dk63.

Jang’ombe Boys; Hashim Ruga, Shomary Ismail, Muharami Issa, Ibrahim Said/Abubakar Ali dk72, Ali Badru, Yakoub Omar, Abdi Kassim, Khamis Makame, Hafidh Juma, Juma Ali/Ali Suleiman dk67 na Abdulsamad Ali.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM