
Serikali imezitaka shule zote za msingi na sekondari binafsi
zilizowafukuza ama kuwataka wazazi na walezi kuwahamishia watoto wao
shule zingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kuwarudisha
mara moja shuleni bila masharti yoyote.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Nicolas Buretta kupitia taarifa yake kwa vyombo
vya habari ambayo imeeleza kuwa wizara hiyo imebaini kuwepo kwa shule
zisizo za serikali na hasa zinazomilikiwa na mashirika ya dini
zilizokiuka utaratibu wa elimu nchini kwa kufanya matendo hayo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa shule hizo pia zimeendelea kukaririsha,
kuhamisha shule nyingine darasa au kuwafukuza wanafunzi hao katika shule
kwa kigezo hicho.
“Wazazi na walezi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu
hizo, wahakikishe wanawarudisha watoto wao kwenye shule walizokuwa
wakisoma ili waendelee na masomo kama kawaida,” ilieleza sehemu ya
taarifa hiyo.
Aidha wizara hiyo imeendelea kuzitaka shule hizo kuwa na utaratibu wa
kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo badala ya
kukaririsha darasa kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa
na shule, na kwamba ikitokea ulazima wa kufanya hivyo taratibu zilizopo
zifuatwe.
Wizara hiyo imeongeza kuzitaka shule zote zilizowataka wazazi na
walezi kuwahamishia watoto wao katika shule nyingine kwa kigezo cha
kutofikia wastani wa ufaulu wa shule kufuta agizo hilo na kuendelea na
wanafunzi hao bila masharti yoyote.
BY: Emmy Mwaipopo
No comments:
Post a Comment