Sunday, 8 January 2017

Ripoti Mpya Ya Mashirika Ya Kijasusi Marekani Yadai Rais Putin Wa Urusi Aliingilia Uchaguzi Wa Marekani

Ripoti mpya iliyotolewa na mashirika ya kijasusi nchini Marekani Ijumaa wiki hii imedaiwa kumtaja Rais Vladimir Putin wa Urusi kuwa aliagiza kufanyika kampeni maalumu kupitia katika vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kufanya udukuzi kwa lengo la kuingilia uchaguzi wa Rais wa Marekani uliofanyika Novemba mwaka jana.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa Rais Putin alifanya hivyo kwa makusudi akilenga kumdhoofisha kisiasa mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton katika kampeni zake za kuwania kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

Maafisa wa mashirika hayo ya kijasusi ya Marekani walitoa kurasa 25 za ripoti hiyo kwa umma Ijumaa wiki hii baada ya kuwa tayari wamewasilisha ripoti ndefu kuhusiana na uchunguzi huo kwa Rais Barack Obama, Rais Mteule Donald Trump pamoja na wabunge waandamizi nchini humo.

Aidha ripoti hiyo inaeleza kuwa Rais Putin na serikali ya Urusi walionyesha upendeleo maalumu kwa Rais Mteule Donald Trump. Hata hivyo licha ya ripoti hiyo kuwekwa wazi Trump bado ameendelea kutetea uhalali wa kuchaguliwa kwake.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM