Friday, 6 January 2017

RC- Walimu marufuku biashara ya bodaboda

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack ameelezea kusikitishwa na tabia ya baadhi ya walimu mkoani hapa kugeukia biashara ya kuendesha bodaboda badala ya kufundisha, akisema hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha taaluma kwa wanafunzi na kuwafanya wasifaulu masomo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa, walimu wengine wamekuwa wakikacha kufundisha na kujihusisha na upigaji picha mitaani.

Aliwaonya na kusema atakayebainika akiendelea kufanya shughuli hizo badala ya kufundisha, atafukuzwa kazi mara moja.

Aliyasema hayo mbele ya Waratibu elimu kata, wakuu wa shule za manispaa na maofisa elimu baada ya kupokea taarifa kuwa baadhi ya walimu mkoani Shinyanga wamekuwa watoro kazini kutokana na kwenda kufanya shughuli binafsi ikiwamo ya kuendesha bodaboda.

Kikao hicho kililenga kuwahamasisha walimu kuongeza juhudi za ufundishaji mwaka huu mkoani Shinyanga.

“Wakuu wa shule naombeni taarifa sahihi za walimu ambao hawafundishi, wanaokwenda kufanya biashara za bodaboda na kupiga picha za mnato, ili Serikali iwashughulikie. Wachague kazi moja wanayoitaka na siyo kukwamisha juhudi za Rais John Magufuli za kukuza kiwango cha elimu nchini,” alisema Telack.

Aliwaagiza wakuu wote wa shule kuacha kutoa ruhusa za hovyo kwa walimu badala yake wawabane ili wafundishe wanafunzi na kuongeza ufaulu.

Pia aliwataka wakuu hao kuandaa daftari la walimu kusaini mahudhurio mara mbili, wakati wa kuingia shuleni na wakati wa kutokao.

Mmoja wa wakuu wa shule aliyehudhuria kikao hicho, Aden Mwakatange wa sekondari ya Mwamalili, alisema suala la walimu kujihusisha na uendeshaji bodaboda linashusha ufanisi wa kazi hasa inapotokea biashara hiyo inafanyika hadi usiku, kwani mwalimu akiingia darasani anakuwa na uchovu kutokana na kuchelewa kulala.

Naye Ofisa Elimu wa Sekondari katika Manispaa ya Shinyanga, Victor Emmanuel alikiri baadhi ya walimu kujihusisha na biashara hizo za bodaboda, upigaji picha za mnato na kubainisha kuwa alishazuia walimu kufanya shughuli zao muda wa masomo, lakini hukaidi, hivyo atawashughulikia.

Chanzo: habarileo.co.tz

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM