Thursday, 12 January 2017

Mke wa Bilionea Msuya Aomba Mahakama imwachie huru

http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2016/09/MSUYa.jpg
Mke wa bilionea Erasto Msuya (marehemu), Miriam Mrita na mwenzake wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, iwaachie huru kwa kuwa hakuna hati ya mashtaka inayowashikilia mahakamani hapo.

Miriam na mshtakiwa mwenzake, Revocatus Muyela, waliwasilisha ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Godfrey Mwambapa, kupitia kwa wakili wao, John Mallya.

Wakili Mallya aliwasilisha ombi hilo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuiomba mahakama iwape muda ili watekeleze amri, iliyowataka wabadilishe hati ya mashtaka. Hivi karibuni mahakama ilitoa siku mbili kwa upande wa Jamhuri, kubadilisha hati ya mashtaka, kwa kuwa ilibaini hati hiyo ilikuwa na mapungufu.

Baada ya wakili Kishenyi kuomba aongezewe muda wa kurekebisha hati, Mallya alidai amri ya mahakama ni sheria na kama hawatekeleza sheria hiyo, hakuna hati yoyote inayowashikilia washtakiwa hao, hivyo aliomba waachiwe huru.

Hata hivyo, Kishenyi alidai kuwa hawajakataa kutekeleza amri ya mahakama, lakini wanaomba muda, pia wanaweza kuiarifu mahakama kama wanakata rufaa au la. Aidha aliiomba mahakama isikubali ombi la washtakiwa, bali iendelee kuwashikilia kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Mwambapa aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 23, mwaka huu ili aweze kutoa uamuzi wa hoja hizo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa Mei 25 mwaka jana katika eneo la Kibada wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa makusudi walimuua Aneth Msuya kwa kumchinja akiwa nyumbani kwake.

Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni mke wa aliyekuwa kaka wa Aneth, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama bilionea Msuya.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM