Friday, 9 December 2016

UTAFITI MPYA HII NDIO IDADI YA WANAUME WANAOPIGWA NA WAKE ZAO,WANAUME 45 WADAI KUPIGWA NA WAKE ZAO

WANAUME 45 walio kwenye ndoa wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa wamevunja ukimya wakidai kupigwa na kutelekezwa na wenzi wao, imebainika.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Polisi Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Nkasi, Anna Kisima katika kikao kilichoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Plan International Tanzania kupitia mradi wake wa kuzuia ndoa za utotoni, kilichoketi jana mjini Namanyere.
Kikao hicho kiliwakutanisha viongozi 26 wa dini na viongozi wa kimila 26 na viongozi wa Jeshi la Polisi wilayani Nkasi, ambao walijadiliana haki za mtoto na wajibu wa mwanamke na athari za ndoa za utotoni.
Kisima alisema katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka huu, dawati hilo lilipokea na kutatua migogoro 230 ya ndoa, ambapo mashauri 45 yalikuwa ni malalamiko ya wanaume kupigwa na kutelekezwa na wenza wao.
“Kati ya wanaume hao 45 waliofika kwenye dawati watano walilalamika kupigwa na kunyanyaswa na wake zao huku 40 walidai kutengwa na wenza wao wa ndoa …..miaka ya nyuma wanaume walikuwa wakiona soni sasa wameanza kuvunja ukimya wanaweza kuzungumza bila aibu wala woga,” alisisitiza.
Kuhusu ndoa za utotoni, Kisima alikiri kuwa tatizo hilo ni kubwa wilayani humo, ambako wasichana wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 12 wanaozeshwa kwa lazima na waoaji walitoa mahari ya ng’ombe nyingi.
Akichangia Mratibu wa mradi huo, Nestory Frank alisema Shirika la Plan International Tanzania liliamua kufanya kampeni ya kuzuia na kupambana na dhidi ya ndoa za utotoni katika Wilaya ya Nkasi kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya ndoa za utotoni.
Alisema Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2012 nchini ilionesha kuwa wasichana 20 kwa kila wasichana 30 wameozeshwa wakiwa na umri wa miaka 18.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nkasi, David Mtasya alisema Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata wazazi na wanaume wanaoozesha na kuoa watoto wadogo kwa kuwafungulia kesi mahakamani.
Wakichangia, Mchungaji wa Kanisa la Moravian kijijini Mtenga, Enock Mapori na Yatima Ntalyaga walieleza kuwa mimba za utotoni ni janga la kitaifa. Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na wilayani Nkasi unatekelezwa katika kata za Mtenga, Mkwamba, Nkandasi na vijiji vyake vyote.
HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM