Monday, 26 December 2016

Picha:Rais Magufuli na mkewe walivyoshiriki ibada ya Krismasi mkoani Singida

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli, leo tarehe 25 Desemba, 2016 wameungana na waumini wa Jimbo Katoliki la Singida kusali Misa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatatifu wa Yesu Mjini Singida.

Misa hiyo Takatifu ya Krismasi imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida Mhashamu Edward Mapunda.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri ya Krismasi waumini wote wa Jimbo la Singida na Watanzania wote kwa ujumla na amewasihi kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu kwa kuendeleza amani na upendo na kuacha vitendo vya kubaguana kwa misingi ya dini, kabila, itikadi na kanda zao.

Dkt. Magufuli amewahimiza Watanzania wote kuongeza juhudi katika kuchapa kazi kama alivyofanya Bwana Yesu na pia amesema kwa kuwa maeneo mengi ya nchi yameonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua, ni vema wakatumia vizuri mvua chache zinazoendelea kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili kuepuka upungufu wa chakula.

Kwa upande wa Mkoa wa Singida ambao ni maarufu kwa kilimo cha alizeti, Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda ambayo nchi inatoa kipaumbele kwa kuzalisha alizeti kwa wingi ili zitumike kuzalisha mafuta ya kupikia kwa wingi.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Singida
25 Desemba, 2016

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM