Monday, 19 December 2016

MWANAMKE ALIYESHAMBULIWA KUTOKANA NA ULEMAVU WAKE KWENYE MTANDAO AJITETEA


Mwanamke ambaye picha yake imekuwa ikiongezwa maneno na ujumbe wa utani na kusambazwa mtandaoni kwa sababu ya muonekano wake, amewashambulia wanaotumia picha hizo na kumcheka.

Lizzie Velasquez, 27 anayetoka Austin, Texas hutoa mihadhara ya kuwahamasisha watu na amewahi kutoa hotuba katika kipindi cha TED.

Aidha, ana wafuasi wengi sana mtandaoni.

Alizaliwa na tatizo nadra sana la kiafya ambalo huufanya mwili wake kushindwa kuhifadhi mafuta.

"Naandika ujumbe huu sio kama mwathiriwa lakini kama mtu anayetumia sauti yake.

"Haijalishi muonekano wetu au kimo chetu, unene au wembamba wetu, mwisho wa yote, sisi ni binadamu," aliandika kwenye Instagram.

Kando na picha za Lizzie, wanaosambaza ujumbe wa mzaha mtandaoni ukiwa kwenye picha, ambazo hufahamika kwa Kiingereza kama 'meme', wamekuwa pia wakitumia picha za wanawake wanene, wazee au watu wenye ulemavu.

"Nawaomba mzingatie hilo wakati mwingine mnapotazama picha kama hizi zikisambazwa sana mtandaoni za mtu ambaye hamumfahamu," alisema.

"Wakati huo, huenda ukadhani ni jambo la kuchekesha lakini kwa binadamu aliyewekwa kwenye picha hiyo, labda hisia alizo nazo ni kinyume kabisa."
Kando na mwili wake kushindwa kuhifadhi mafuta, Lizzie pia ana matatizo mengine ya kiafya.

Ana ugonjwa unaoitwa Marfan Syndrome, ambao huathiri urefu wa mikono na miguu ya mtu pamoja na umbo la mwili.

"Naandika ujumbe huu kukiwa usiku sana kama ujumbe wa kukumbusha watu kwamba kuna watu wasio na hatia ambao huwekwa kwenye picha hizi ambao pia hukaa macho usiku wakiangalia kwenye Facebook na kuhisi jambo ambalo siwezi hata kumtakia adui wangu mkuu," aliandika kwenye Instagram.

Ujumbe wake umesambazwa sana kwenye Facebook na Instagram na watu watu wengine.

Kuna uwezekano kwamba ukurasa wa mojawapo ya makundi yanayoeneza picha hizi umefungwa na Facebook baada ya watu wengi kulalamika.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM