Saturday, 31 December 2016

MFAHAMU MKE WA RAIS ALIYEMUWEKEA ‘LIMBWATA’ MUME WAKE RAIS NA KAMPELEKA PUTA AKIWA MADARAKANI

Image may contain: 2 people, hatNdimi Luqman Maloto.
 Yanapotajwa majina ya wake wa marais wa Marekani (US First Ladies), wenye akili nyingi kuwahi kutokea na waliojishughulisha kijamii na kazi zao kuwabeba waume zao, Florence Mabel Harding huwa hatajwi.

Wanaotajwa ni aliyekuwa Mgombea Urais wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu 2016, kwa tiketi ya Chama cha Democrats, Hillary Rodham Clinton ambaye ni mke wa Rais wa 42 wa taifa hilo, Bill Clinton.

Yupo mke wa Rais wa 32, Franklin Roosevelt, Eleanor na Abigail Adams, ambaye ni mke wa Rais wa Pili wa Marekani, John Adams, vilevile mama wa Rais wa Sita wa nchi hiyo, John Quincy Adams.

Wengine ni Jacqueline Kennedy, mke wa Rais wa 35, John Kennedy, Claudia Alta Johnson ‘Lady Bird Johnson’, mke wa Rais wa 36, Lyndon Johnson pamoja na First Lady wa sasa wa nchi hiyo, Michelle Obama.

Katika orodha humuoni Florence lakini kwa vipimo vyote ndiye mke wa Rais wa Marekani, aliyeitikisa Ikulu ya nchi hiyo, White House kuliko wengine wote. Zaidi inaaminika ndiye First Lady aliyekuwa na akili nyingi kupita wote.

Florence aliitumia White House kutimiza matakwa yake kuliko hata mume wake, Rais wa 19 wa nchi hiyo, Warren Gamaliel Harding. Kwamba Rais Harding alizidiwa akili na Florence kwa mambo mengi.

Zipo hotuba, ikiwemo ile ya kuapishwa kuwa Rais wa Marekani, aliyoitoa Machi 4, 1921, ilielezwa kuwa ziliandikwa na Florence. Vyombo vya habari Marekani, viliamini kuwa Florence alikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika hotuba zenye ushawishi kuliko Rais Harding.

Ni kwa sababu hiyo, Florence alikuwa na ushawishi mkubwa na upo uamuzi ambao ulifanywa na Rais Harding lakini vyombo vya habari na wapinzani wa kiongozi huyo, walibeza kwa maelezo kuwa ni maagizo ya First Lady (Florence).

Katika mazingira hayo, Rais Harding alishambuliwa kuwa alikuwa akipelekwa puta na Florence akikosa namna ya kujipambanua kuwa yeye ndiye mume na ndiye Rais, kwamba mke wake alikuwa na msuli mkubwa kuliko mume.

Kwetu Tanzania hasa uswahilini tunapoishi, mwanamke anayechomoza na kutoa uamuzi kuliko mume au anayekuwa na vitabia visivyofaa halafu mume wake anakuwa hawezi kumdhibiti, huwa inasemwa mwanaume huyo amelishwa limbwata.

Kwa msingi huo, Rais Harding kama angekuwa Mtanzania, hata kama vyombo vya habari visingeandika au asingeshambuliwa waziwazi japo na wapinzani wake, basi hata minong’ono ya chini ingekuwepo; Rais wetu kalishwa limbwata.

Tafsiri ya limbwata ni dawa za kimazingara ambazo inadaiwa mwanaume akilishwa anakuwa zoba, kwa hiyo baada ya hapo mke anaweza kufanya anavyotaka na mume asiwe na kauli. Mwanaume wa hivyo mara nyingi huitwa bwege, yaani mwanaume aliyezubaa na anayetia aibu.

VITIMBI VYA FLORENCE HARDING

Florence unaweza kumwita First Lady wa Ma-First Lady, maana ni wa kwanza kwa kila kitu. Alikuwa mke wa kwanza wa Rais wa Marekani, kuandaa sherehe za mara kwa mara White House, alialika watu kwa chakula cha jioni na kuwaburudisha kwa kutazama filamu baada ya chakula.

Alikuwa na utaratibu wa kualika mcheza filamu mkubwa Ikulu na kula naye chakula, iwe cha mchana au jioni. Alifanya hivyo alivyojisikia na Rais Harding hakuwa na ubavu wa kupingana na hilo.

Ni First Lady wa kwanza kucheza filamu mume wake akiwa Rais. Kipande ambacho alicheza ni cha utangazaji wa taarifa ya habari. Alifanya hivyo kwa sababu alipenda sana taaluma ya uandishi wa habari na aliifanyia kazi kama mwekezaji kupitia kampuni ya Rais Harding.

Florence alikuwa na tabia ya kujibu barua za Rais na kutoa maelekezo bila mume wake kujua. Baada ya kufanya hivyo, alimjulisha mume wake kuhusu uamuzi ambao aliufanya kwa niaba yake kupitia barua zenye nembo na mhuri wa Rais wa Marekani.

Alikuwa akiandaa sherehe (party) mara kwa mara ndani ya boti la Rais wa Marekani na kuwaalika watu kusherehekea pamoja naye. Sherehe hizo zilifanyika usiku na mchana ndani ya boti.

Kwa uamuzi wake mwenyewe, Florence alikuwa akiwaalika waandishi wa habari na kuwafanyia tafrija ya siri Ikulu, akila na kunywa nao. Alifanya hivyo kuhakikisha anawaweka karibu, wawe wanampamba kuwa yeye ni First Lady bora kuwahi kutokea, vilevile kuuzungumzia vizuri utawala wa mume wake.

Florence alikuwa mke wa Rais wa Marekani ambaye alikuwa na utaratibu wa kufanya mikutano na waandishi wa habari pamoja na kulihutubia taifa mara kwa mara kuliko mume wake.

Akitaka kujua kila kitu kwenye jamii na ndani ya Serikali ya mume wake, Florence wakati mwingine alijifanya shushushu, vilevile alitoa maelekezo kwa taasisi za ujasusi ili zimtafutie alichotaka.

Vitimbi vya Florence haviishii hapo, kingine ni kuwa aliamini sana ushirikina, wakati mwingine aliwaalika Ikulu wapiga ramli na wanajimu (fortunetellers and astrologers) na kuwataka wambashirie mambo yajayo, vilevile wamweleze mambo ya giza ambayo yalikuwa yakimzunguka.

Mshangao mkubwa ni pale Florence alipompa mafunzo mbwa wake pendwa ya kupokea na kujibu barua. Yote hiyo ni kwa sababu alimwamini mno mbwa wake.

Kitabu kilichaondikwa na mwandishi Carl Sferrazza Anthony, kinachotwa Florence Harding (The First Lady, the Jazz Age, and the Death of America's Most Scandalous President), ndani yake yameelezwa mengi kuhusu Florence.

FLORENCE ALIMPA HARDING URAIS
Baniani mbaya kiatu chake dawa. Florence alicheza nafasi muhimu kumfanya mume wake kuwa Rais, wakati mwanzoni alionekana mgombea dhaifu. Kipengele hiki ndicho ambacho kinatoa tafsiri ya kwa nini Florence alikuwa na sauti kuliko mume wake baada ya kushinda urais.

Harding alikuwa mgombea dhaifu katika mbio za kuwania tiketi ya Chama cha Republican, kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka 1920. Baada ya kujiona hatoshi alichukua uamuzi wa kujitoa.

Ni Florence aliyemnyang’anya Harding simu, alipokuwa anampigia kampeni meneja wake, Harry Daugherty kumweleza dhamira yake ya kujitoa. Florence alimwambia: “Unataka kufanya nini? Kujitoa? Huwezi kujitoa mpaka mkutano mkuu wa taifa wa chama ufanyike na upite.”

Baada ya hapo Florence alikata simu. Harding ilibidi asalimu amri kwa mke wake, akamwambia: “Sawa, basi nisaidie kuwambia Harry Daugherty kuwa tutapambana mpaka barafu la Jehanamu liyeyuke.”

Sababu ya Harding kutaka kujitoa, ilikuwa ni matokeo ya awali kuonesha kushindwa hata katika ngome zake muhimu. Harding alikuwa na uhakika angepata kura 48 za jopo katika Jimbo la Ohio, lakini alipata 39 na kura za jumla 15,000 tu. Indiana ambayo palikuwa pia tegemeo lake alikamata nafasi ya nne.

Mwaka 1920 ulikuwa wa bahati kwa Harding, kwani aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda tiketi ya Republican, alikuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo kati ya mwaka 1901 mpaka 1909, Theodore Roosevelt, aliyekuwa anataka kuongoza taifa hilo kwa kipindi cha tatu.

Hata hivyo, Roosevelt alifariki dunia ghafla Januari 6, 1919, hivyo kuacha mlango wazi. Walijitokeza ni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Marekani, Leonard Wood, aliyekuwa Gavana wa Illinois, Frank Lowden, Seneta wa California, Hiram Johnson, Rais wa baadaye wa nchi hiyo, Herbert Hoover, Gavana wa Massachusetts, Calvin Coolidge, Jenerali John Pershing na Harding.

Desemba 17, 1919, Harding alipotoa tangazo la kuwania tiketi ya kuwa mgombea urais kupitia Republican, watu walimwona kama anakwenda kusindikiza. Na kweli matokeo ya jumla yalipotoka, kuelekea mkutano mkuu wa chama, Harding alikuwa wa sita kwa kura.

Florence alitumia gazeti lao la familia, linaloitwa The Marion Star kumpamba mume wake na kuwashambulia wapinzani wake. Florence pia ndiye aliyemsaidia Harding alipogombea useneta wa Ohio mwaka 1914 na kumwewezesha kushinda. Alimsaidia katika usimamizi wa fedha na mvuto wa kijamii.

Hii ni kwa sababu Florence alikuwa maarufu na jina lake lilitosha kumwombea kura mume wake. Hvyo basi, kama ambavyo alimsaidia Harding kushinda useneta wa Ohio, ndivyo jina lake lilivyombeba Harding katika mbio za urais.

Baada ya Harding kutoka wa sita, walielekea kwenye mkutano mkuu wa taifa (1920 Republican National Convention). Ghafla hali ya hewa ilichafuka, mgawanyiko mkubwa ulitokea. Kashfa ya watu kutumia fedha kununua wajumbe ilirindima.

Ukafuata uchunguzi ambao ripoti yake ilipokamilika, ilibainisha kuwa Wood alitumia Dola1.8 milioni ambazo kwa sarafu ya sasa ni Sh4 bilioni. Lowden alitumia Dola600,000 (Sh1.3 bilioni), Johnson Dola194,000 (Sh400 milioni), Harding alionekana kutumia kiasi kidogo zaidi, Dola113,000 (Sh227 milioni).

Florence aliitumia ripoti hiyo kuwaonesha wagombea wengine kuwa wananunua urais. Kampeni kubwa ikawa inafanywa kuwa Harding awe mgombea kwa sababu ndiye aliyetumia fedha kidogo kuliko wengine.

Juni 11, 1920, kura za mkutano mkuu zilipigwa lakini hakuna hata mmoja aliyefikisha kura 498 zilizohitajika ili atangazwe mgombea. Wood alipata 314, Lowden 289 na Harding alipata 65.

Usiku wa Juni 11 mpaka 12, 1920, historia iliandikwa, pale wazee wa chama (party elders) walipojitokeza kuwalazimisha wajumbe wa mkutano mkuu wa Republican kumchagua Harding ili kukitetea chama kisigawanyike.

Kutokana na shinikizo la wazee, wajumbe wa mkutano kwa kura nyingi walimchagua Harding kuwa mgombea urais wa Republican. Tukio ambalo liliweka historia kwa sababu hakuwa amefikiriwa kabla.

Shukurani za ushindi huo zinakwenda kwa Florence ambaye mbali na gazeti lake kutumika kuchafua wagombea wengine pamoja na kumpamba Harding, vilevile alipenya kwa watu muhimu kwenye chama na kuwashawishi wazee kumkubali Harding.

FLORENCE NA HARDING WALIVYOKUTANA
Florence alikuwa mkubwa kwa Harding kwa miaka mitano. Florence alipofunga ndoa na Harding, ilikuwa ndoa yake ya pili. Mwaka 1880, Florence akiwa na umri wa miaka 20, aliolewa na mume wake wa kwanza, Henry DeWolfe na kuzaa naye mtoto mmoja wa kiume. Mwaka 1886 waliachana.

Mwaka 1891 alifunga ndoa na Harding. Wakati huo, Harding alikuwa mjasiriamali, akimiliki gazeti The Marion Star. Baada ya ndoa yao, Florence alishika nafasi ya uongozi wa gazeti hilo na ndipo lilianza kupata mafanikio kwa kuchapa nakala nyingi.

Baada ya kushika uongozi wa gazeti hilo, ndipo Florence alipodhihirisha uwezo wake wa kuongoza gazeti, umaarufu wake binafsi ulipaa zaidi, vilevile umaarufu wa gazeti uliongezeka.

Umaarufu wa Florence ulikuwa mtaji mkubwa kwa Harding baada ya kuteuliwa na Republican, kwani mwanamke huyo alifanya kampeni ya nguvu. Yalikuwepo maneno kwamba Harding alishinda urais si kwa sababu nyingine, bali kuwa mume wa Florence.

KIFO CHA WARREN HARDING

Wakati mchakato wa Republican ulipoanza, Harding akionekana kuwa mgombea dhaifu, aliyekuwa mtabiri maarufu wa Marekani, Madame Marcia Champrey, alimtabiria Harding kushinda urais lakini akasema pia kuwa angekufa kabla ya kumaliza muhula wake mmoja wa miaka minne.

Agosti 2, 1923, Harding alifariki dunia baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka miwili na nusu. Kifo cha Harding kilijaa utata mkubwa. Ikavumishwa kuwa Florence alimpa sumu Harding kwa sababu za wivu wa mapenzi.

Msimamo wa Florence kukataa mwili wa Harding usifanyiwe uchunguzi kubaini kilichomuua, ulisababisha maneno mengi zaidi kuwa alimpa sumu baada ya kubaini ana uhusiano na mwanamke mwingine.

Florence alipokataa mwili wa mume wake usifanyiwe uchunguzi, alikuwa akisisitiza watu kuheshimu utabiri wa Madame Marcia kuwa Harding angeshinda urais kisha angekufa akiwa madarakani.

Baadaye Florence alishambuliwa kama mwanamke muuaji, wapo walioandika kuwa anaweza kuwa First Lady mwenye roho mbaya kuliko wote kuwahi kutokea Marekani.

Hata hivyo, Florence hakufikishwa mahakamani, taarifa zilidai alikufa kwa shambulio la moyo, zipo nyingine zilieleza ni sumu.

Baada ya kifo cha Harding, Florence aliishi mwaka mmoja na miezi mitatu tu, kwani Novemba 21, 1924, naye alifariki dunia. Yote yasemwe lakini Florence anaendelea kuwa mwanamke maarufu, aliyemuingiza mume wake Ikulu, kisha akaitumia White House kama nyumbani kwake, japo kilikuwa kipindi cha miaka miwili na nusu tu.Chanzo/ www.luqmanmaloto.com,

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM