Friday, 23 December 2016

MASWALI 5 YA AJALI ZA MBUNGE SUGU TANGU AINGIE BUNGENI

  
Na Sifael Paul | Gazeti la Amani, Toleo la Desemba 22, 2016
MBEYA: Kufuatia kuandamwa na ajali za mara kwa mara ndani ya kipindi chake cha ubunge yapata miaka sita sasa tangu mwaka 2010, Mbunge wa Mbeya Mjini kwa leseni ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Othman Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu (pichani) ameibua maswali matano.
Baadhi ya wakazi wa Mbeya mjini waliozungumza na Amani walionesha wasiwasi wao hasa kwa imani mbaya kwamba, huenda kuna wabaya wa mbunge wao wanaisaka roho yake kwa njia hiyo.
“Mheshimiwa Sugu sasa ajali kwake zinataka kuwa jambo la kawaida. Lakini sisi tuna wasiwasi kwamba, kuna wabaya wake wanaisaka roho yake. Kama wapigakura wake tunamwelekeza kusali sana na kutoa sadaka mbalimbali. Itamfukuzia ajali hizi,” alisema mzee Mwakatobe, mkazi wa Ghana, Mbeya.
 
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Othman Mbilinyi ‘Sugu’ (pichani kushoto). Picha zote na maktaba.
Naye mzee Ima Mwakalindila akizungumzia ajali za mbunge huyo alisema:
“Hee! Hii ya juzi ndiyo nilishangaa sana. Mpaka ikaua mtoto! Sasa najiuliza maswali kama matano hivi. Hizi ajali ni kwa ajili ya Sugu tu? Je, yeye ameshafanya juhudi gani na Mungu wake kushughulika na ajali hizi? Je, madereva wake wana uzoefu kidogo? Japo mimi siamini kama wana uzoefu kidogo, maana yeye ni mbunge lazima atakuwa anaajiri madereva makini.
“Lakini swali langu lingine kwake ni je, ukoo wake una kawaida ya matambiko? Na ameyafanya? Maana kuna koo ambazo kama hazifanyi tambiko mizimu inasumbua sana kwa kuleta ishara nyingi mbaya.
“Lakini swali langu la tano kuhusu hizi ajali ni kwamba, zinatokea tu kwa bahati mbaya au zinapangwa na mtu? Maana nina wasiwasi kuwa, huenda kuna watu wanamtengenezea ajali bila mwenyewe kujua.”
Mpaka sasa, Sugu ameshapata ajali nne na ajali hizo zimemtokea kama ifuatavyo:
AJALI YA KWANZA
Jumamosi ya Januari 14, 2012, gari la Sugu aina ya Toyota Land Cruiser Amazon, liliwaka moto likiwa eneo la Kibaha Kwamatiasi, Pwani. Ndani yake, mbali na Sugu, alikuwemo Mbunge wa Mbozi Mashariki (Chadema), Joseph Silinde.
AJALI YA PILI
Juni 19, 2013, Sugu alipata ajali katika eneo la Kasheki wilayani Hanang’ akielekea Arusha mjini kuungana na wabunge wengine wa Chadema katika shughuli ya kuaga marehemu waliolipukiwa na bomu kwenye mkutano wa Chadema.Katika ajali hiyo hakuna mtu aliyejeruhiwa lakini gari la Sugu liliharibika vibaya baada ya kugongana na basi la abiria.
 

Gazeti la Amani, Toleo la Desemba 22, 2016
AJALI YA TATU
Januari 10, 2015, iliripotiwa kuwa, Sugu alinusurika katika ajali ya gari eneo la Mlima Kitonga, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Chanzo cha ajali hiyo kilitajwa kuwa ni kufeli kwa breki, hali iliyosababisha gari lake kuanguka ‘kichwa chini miguu juu’ wakati mbunge huyo akitokea Mbeya kuelekea Mikumi mkoani Morogoro kwenye mkutano wa hadhara.
Katika gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser ambalo lilikuwa likiendeshwa na Mheshimiwa Sugu, lilikuwa limebeba watu wanne ambao wote walisalimika na kutoka salama licha ya michubuko ya mkononi aliyoipata Sugu.

AJALI YA NNE
Desemba 17, 2016, Sugu alipata ajali kwenye kivuko cha barabara (zebra) ambapo gari lake lilimgonga mtoto mwenye umri wa miaka 15 ambaye alifariki dunia wakati akipelekwa hospitalini.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa mbili asubuhi katika eneo la Iyunga jijini Mbeya, wakati gari la Sugu likiwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Songwe kwa ajili ya mapokezi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye hata hivyo hakutokea.
Juzi, Amani lilimpigia simu Sugu ili kumsikia anasemaje kuhusiana na ajali hizo lakini iliita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM