Monday, 12 December 2016

KWA NINI MIPANGO YAKO YA MAENDELEO IMEKWAMA 2016?? MAJIBU YANAWEZA KUWA NI HAYA

 
Wakati ikiwa zimebaki siku chache kumaliza mwaka 2016, ni vizuri kujiuliza maswali kadhaa kabla ya kuanza mwaka mpya 2017, je mipango uliyokuwa umejiwekea kiuchumi umeitekeleza? Umefanikiwa au ulipata hasara?

Majibu ya maswali hayo ndiyo yanayoweza kukupa dira wakati unapoanza mwaka 2017.

Wachunguzi wa mambo wanasema asilimia tatu ya watu duniani wanamalengo wakati asilimia 97 hawana malengo hivyo lolote likitokea wakati wowote, na wao hukurupuka kulifanya na mara zote mafanikio yao huwa ni kwa bahati.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Dk Rwekaza Chachage alisema zipo sababu nyingi zinazoweza kuwafanya watu wasifanikiwe kwenye mipango yao wanayojiwekea mwanzo wa mwaka, ikiwamo kukurupuka katika kuweka mipango mingi bila kuwa na mikakati ya kuitekeleza wala kujua vipaumbele.

“Haiwezekani mipango yako yote uliyoiweka mwanzo wa mwaka ukaipa vipaumbele, usiwe na mipango mingi, panga michache na ipatie vipaumbele,” alisema Dk Chachage.

Alisema watu wengi wamejikuta wakimaliza mwaka bila kutekeleza mipango yao kutokana na matumizi mabaya ya muda.

“Wanadamu wote tuna saa 24, hivi umeshawahi kujiuliza unatumiaje muda katika kuleta faida kwenye maisha yako? Usitumie muda mwingi kwa mambo yasiyo ya msingi, muda ni hazina ambayo ikishapotea hairudi,”alisema.

Alisema pia upo ugonjwa wa kuahirisha ambao umekuwa ukiwatesa wengi na kujikuta wanamaliza mwaka bila kutekeleza mipango yao.

Aliwashauri watu kuwa na uwezo wa kusema ‘hapana’ wanapokutana na marafiki, ndugu au jamaa ambao watataka kutumia muda wao kwa ajili ya manufaa yao wenyewe.

Alisema wapo baadhi ya watu ambao hupenda kuwaridhisha wengine kwa kushindwa kukataa yale wanayoambiwa kuyafanya hata kama yatachangia kuvuruga mipango waliyokuwa wamejiwekea kwenye ratiba.

Dk Chachage alisema ni vizuri kuwa na mipango michache unayoweza kuitekeleza kiufasaha kutokana kuliko lundo la mipango ambayo kamwe huwezi kuikamilisha.

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omary Mbura alisema mabadiliko ya utawala pia yamechangia baadhi ya watu kushindwa kutimiza mipango yao ya mwaka.

Alisema katika utawala uliopita wa awamu ya nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete kulikuwa na mianya mingi ya kupata fedha ambayo hivi sasa haipo tena jambo linalowalazima waliokuwa wamejiwekea mipango wakitarajia fedha hizo, kujipanga upya.

“Mie mwenyewe kuna baadhi ya vikao nilikuwa nalipwa, lakini utawala huu unanifanya nifikirie zaidi namna ya kufanikisha mipango yangu kwa kipato cha sasa, kiufupi ni kwamba Serikali hii inatushape tujipange upya,” alisisitiza.

Halikadhalika alisema wapo baadhi ambao hawakuipanga vizuri mipango yao kwa kutolenga kile wanachotaka kufanya na hivyo kujikuta wanamaliza mwaka bila kutekeleza.

“Mtu anaema tu anataka kujenga, wapi? Nini? Unapaswa kupanga malengo yako ya mwaka kulingana na raslimali zilizopo usitafsiri ndoto ukaweza kwenye mipango, hutafikia mafanikio,” alisema.

Dk Mbura alisisitiza mipango hiyo kutengewa muda maalum, kuisimamia kwa ukaribu na kutoruhusu matatizo mengine yanayojitokeza katikati ya mipango kuiharibu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Christopher Magomba alisema wengi hujiwekea mipango isiyo halisi na hivyo kuwawia vigumu kwenye utekelezaji.

Akitoa mfano alisema unaweza kuwekeza kwenye ardhi kwa maana ya kilimo lakini hujui mkakati upi utakuwezesha kupata fedha wala hujui hali ya hewa itakuwaje, ikiwa vinginevyo mpango huo lazima utafeli.

“Ipo kanuni ya kufanikiwa kiuchumi inayoitwa ‘smart’ kwa maana ya (Specific, Measurable, Realistic and Time oriented), watu wengi hatuweki malengo kwa kufuata kanuni hiyo ndio maana mwisho wa mwaka tunaanza kumtafuta mchawi,” alisema.

Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Norman Sigalla-King alisema kutokuwa na utashi sahihi wa jambo la kiuchumi linalotakiwa kufanyika ni kati ya sababu za kumkwamisha mtu kutofikia malengo yake ya mwaka.

“Tafiti zinaonyesha kuwa watu waliowengi hawatambui mambo wanayoweza kufanya kwa usahihi, wanafanya kazi za kiuchumi kwa kubahatisha tu, ni muhimu mtu kupeleka nguvu kwenye mambo ambayo yako ndani ya uwezo wako, hapa naongelea utashi sio elimu ya vyeti vya darasani,” alisema.

Profesa Sigalla King ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Makete alisema unaweza kuwa na elimu ya darasani upande huu, lakini utashi wako ukawa upande mwingine kwa kuwa inategemea zaidi nini ulikuwa msukumo wa kusoma ulichosoma.

Profesa Sigalla King alisema sababu nyingine ni kutokutumia kiwango cha ufahamu unaotokana na elimu kwa usahihi .

Alisema kimsingi fulsa za maendeleo ya kiuchumi hazizuiwi na kiwango cha elimu cha mtu na kwa kuwa kinachotakiwa ni kutambua kiwango cha elimu ulichonacho na kitu ambacho kwa elimu hiyo unaweza kufanya.

“Kwa hiyo darasa la saba ana fulsa zake, ambaye hakufika darasa la saba lakini anajua kusoma na kuandika pia anazo fulsa zake, vivyo hivyo kidato cha nne, cha sita na hata shahada kwa ngazi mbalimbal,” alisisitiza.

Aidha alisema kubadilika kwa sera kunaweza kufanya mipango ya uwekezaji wa mtu au kampuni kushindwa kufikiwa.

Aliongeza kuwa hiyo inajumuisha madiliko katika kodi, uhitaji wa bidhaa, sera za fedha ikiwa ni pamoja na riba za mikopo kwenye taasisi za fedha.

Sababu nyingine ni maadili ya kutunza mitaji au matumizi ya fedha yasiyo na maadili na kutojifunza kwa waliofanikiwa au hata kwa wenye ufahamu wa biashara unayotaka kufanya kunaweza kukwamisha mipango yako.

“Ni vizuri kila mtu awe na utayari wa kujifunza kwa waliofanikiwa au wenye ueledi katika eneo hilo,” alisisitiza.

Mtaalamu mwingine wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Veronica Msemwa alisema watu wengi wameshindwa kufanikiwa baada ya kukatishwa tamaa na wengine.

Alisema siku zote kukatishwa tamaa ni sumu ya mafanikio katika mipango ya aina yoyote na kwamba, ili kufanikiwa ni lazima kutokubali watu wengine wakuongoze katika mipango mipya ya mwaka ujao, utakayojiwekea.

“Inawezekana wanakuonea wivu, hivyo huna sababu ya kupoteza muda kuwasikiliza wanaoweza kukukatisha tamaa kikubwa ni kusimama kama wewe, na kusonga mbele,”alisema.

Aliwashauri watu kuwa wabunifu kwenye kutengeneza mikakati ya mafanikio kwenye malengo yao

Mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia, Frank John alisema tabia ya baadhi ya watu ya kulalamika hata kwa mambo mema wanayofanyiwa ni moja ya sababu zinazoweza kuwafanya wasifanikiwe.

“Watu hawa ikinyesha mvua watalalamika, jua likiwaka watalalamika na hata watendewe mema kiasi gani bado ni walalamishi tu, ukiwa aina hii usitegemee mafanikio hadi utakapokubali kubadilika,” alisema.

Alisema wengi wameshindwa kwa kutaka kuiga maisha ya watu wengine na kujikuta wakijiingiza kwenye ulevi, starehe na mambo mengine yasiyo ya msingi badala ya kusimamia mipango yao.

Alisema hakuna haja ya kuishi maisha ya watu wengine wakati mipango uliojiwekea mwanzo wa mwaka inahitaji gharama katika kuitekeleza.

“Hapo upo umuhimu wa kuchagua marafiki wanaoweza kukushika mkono na kukuongoza kwenye mafanikio, ukikosea kuwa na marafiki wanaowaza starehe na ulevi muda wote jua huwezi kutekeleza mpango wowote,”alisema.

Alidai kuwa jambo lolote lenye mafanikio linahitaji kujituma na bidii katika kulitekeleza hivyo kuna wakati lazima ukubali kuuchosha mwili, ili kufanikisha mipango yako.

Mbunge wa viti maalum (CCM), Amina Mollel alisema wengi wameshindwa kutimiza mipango yao baada ya kukata tamaa mapema na kukosa uvumilivu.

Alisema ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mafanikio bila gharama ikiwamo matumizi ya muda, raslimali na wakati mwingine, kuuchosha mwili.

“Ukijidanganya ukasikiliza watu wanaweza kukukatisha tamaa ukajikuta mtu wa manung’uniko muda wote, usiruhusu hali hiyo mwaka 2017,”alisisitiza.

Mfanyabishara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Salum Tilwa alisema mipango yake mingi ilishindikana kutokana na mabadiliko ya kiuchumi. MWANANCHI
“Wateja hasa wa nguo walipungua hivyo nilishindwa kufanikisha mpango wangu wa kufungua duka jingine, utawala wa sasa unatufanya tufikirie kubuni vitu vingine vya kutuingizia fedha,” alisema.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM