Tuesday, 20 December 2016

HIVI NDIVYO BALOZI WA URUSI ALIVYOPIGWA RISASI NA KUUAWA


No automatic alt text available.Wizara ya Mambo ya Nje imethibitisha kuwa Balozi wa Urusi, Andrey Karlov amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Ankara, Turkey.
Hatari sana, ngoja tumsikie Rais wa Russia, Vladimir Putin atatoa tamko gani. Tayari wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi kupitia msemaji wake Maria Zakharova imesema tukio hili ni la kigaidi na pia Marekani kupitia msemaji wake John Kirby na mataifa mengine kadhaa tayari wamelaani tukio hilo la leo.Mtu aliyemshambulia balozi , alikuwa amevaa suti na tai akiwa na
muonekano wa ''kama bodyguard'' huku akipaza sauti kwa lugha ya ki-Russia na pia maneno " Aleppo-Syria ", '' Allahu Akbar'' ! alipigwa risasi na polisi mita michache toka eneo la tukio. Katika shambulio hilo wakati wa maonesho ya picha, watu wengine watatu walijeruhiwa na muuaji wa Balozi Andrey Karlov. Pia mshambulizi huyo kwa lengo maalum alivyatulia risasi picha kadhaa na kuziharibu, hii inasemekana ktk kuonyesha ujumbe Fulani dhini ya picha hizo.
Maonesho ya picha aliyohudhuria balozi Andrey Karlov yalikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili za Russia na Turkey. Maudhui ya maonesho hayo yalikuwa kusaidia ''kufahamiana'' zaidi kati ya Russia na Turkey kutokana na mlolongo wa matukio yaliyotia doa ushirikiano ikiwemo tukio la kutunguliwa kwa ndege ya Urusi na majeshi ya Uturuki November mwaka 2015.
Kwa mujibu wa RT (Russian Television) News habari ambazo hazijathibitishwa, Muuaji ametambuliwa kuwa ni ofisa wa Polisi wa Uturuki aliyezaliwa mwaka 1994 na kuhitimu elimu kiwango cha diploma na kujiunga na idara ya Polisi mwaka 2014 na baadaye kutimuliwa kazi mwaka 2016 baada ya mapinduzi ya Turkey kumuangusha Rais Recep Tayyip Erdoğan kufeli mapema mwezi Julai mwaka huu (2016).
Eneo lilipotokea tukio la kigaidi jijini Ankara, Uturuki ni karibu na majengo ya ubalozi ya mataifa ya Marekani, Uingereza n.k ambapo huwa kuna ulinzi mkali kutokana na majengo mengi nyeti.
Balozi Andrey Karlov mbobezi wa kidiplomasia kwa miaka 40, ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Moscow State Institute of International Economic Relations na Chuo cha Kidiplomasia cha the Diplomatic Academy of the Russian Foreign Ministry aliwahi pia kuwa balozi wa Urusi huko North Korea 2001-2006.
Tayari jumuiya ya wana-Diplomasia Urusi wamesema kuwa tukio hili la leo la mauaji ya Balozi Andrey Karlov ,yaweza kuwa limechochewa sana kihisia na matamko ya miezi mingi iliyopita ya wanasiasa wa nchi za magharibi ktk vyombo vya media na propaganda social media : blogs, twitter, facebook, YouTube juu ya hatua za Urusi huko Aleppo, Syria dhini ya wapiganaji wa Free-Syria na uungwaji mkono wa kijeshi wa Urusi kwa utawala wa Rais Bashar al Assad wa Syria.Habari za punde kidogo, Rais Vladmir Putin ametoa tamko na kuwa kamati ya uchunguzi tayari imetumwa Turkey kuungana na vyombo vya Turkey katika uchunguzi wa tukio hili. Pia Putin amethibitisha kuzungumza kwa simu na Rais wa Turkey, Recep Tayyip Erdoğan kuhusu tukio hilo na kukubaliana kufanya kazi pamoja kusaidia kufahamu waliopanga mpango huo wa mauaji ya leo.
Rais Putin amempa sifa kemkem marehemu Balozi Andrey Karlov kwa kazi kubwa wakati wa uhai wake ikiwamo kushughulikia tukio nyeti la utunguaji wa ndege ya Urusi uliotekelezwa na majeshi ya Uturuki. Rais Putin amesema weledi wa balozi huyo ulisaidia tukio hilo la kutunguliwa ndege kumalizika salama kidiplomasia. Putin amesema tukio la leo la mauaji ya Balozi Andrey Karlov, halitafanya Urusi kupunguza wajibu wake kuisaidia serikali ya Syria katika vita vyake na makundi mbalimbali nchini Syria.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM