Sunday, 13 November 2016

Stars yafungwa 3-0 na Zimbabwe

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Charles Boniface Mkwasa amesema timu yake imepoteza kwa bahati mbaya mchezo dhidi ya Zimbabwe huku akitaja magoli mawili ya haraka ya kipindi cha kwanza na kipindi cha pili kuchangia kufanya mchezo kuwa mgumu kwao.
Taifa Stars imepoteza mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa kwa kipigo cha magoli 3-0 ugenini dhidi ya Zimbabwe.

Tanzania ilisafiri kuelekea mjini Harare ikiwa na nyota wake wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi pamoja na wale wanaocheza ligi ya ndani kucheza mchezo wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya FIFA.

Magoli ya Zimbabwe yamefungwa na Knowledge Musona dakika ya 9, Mathew Rusike dakika ya 55 na Nyasha Mushekwi.

Stars ilipata nafasi kadhaa za kufunga lakini haikufanikiwa kukwamisha mpira kambani.

Baada ya mchezo kumalizika, shaffihdauda.co.tz ilifanya mazungumzo moja kwa moja na afisa habari wa TFF Alfred Lucas ili kutaka kujua kocha wa Taifa Stars Boniface Mkwasa amepokeaje matokeo hayo pamoja na kutaja sababu ya timu yake kupoteza mchezo.

Kwa mujibu wa Alfred Lucas, Mkwasa amesema Stars imepoteza mchezo kwa bahati mbaya lakini aina ya magoli yaliyofungwa yaliwachanganya wachezaji.


“Kocha amesema timu imepoteza mchezo kwa bahati mbaya lakini amesema aina ya magoli yalifyofungwa yaliwachanganya wachezaji na kupelekea kupoteza mchezo. Amesema Zimbabwe ilifunga goli la mapema kipindi cha kwanza (dakika ya 9) ambalo liliwachanganya wachezaji na muda mwingi wakawa wanafikiria zaidi kusawazisha,” amesema Lucas akinukuu maneno ya Mkwasa baada ya mechi.

“Kipindi cha pili wakati Stars ikijipanga kusawazisha, ikafungwa tena goli la mapema (dakika ya 55) na kuvuruga mipango yao ya kuhakikisha wanasawazisha.”Kwa mujibu wa Alfred Lucas, Stars inatarajia kurejea nchini kesho saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM