Friday, 9 September 2016

Mambo 3 mjasiriamali mdogo wa Tanzania anaweza kujifunza kutoka kwa Kanye West

Kanye West si ni rapper wa Marekani, ana uhusiano gani na mjasiriamali wa Tandahimba? Ni swali ambalo huenda umejiuliza uliposoma tu kichwa cha habari.
kanye-west-time-100-2015-titans
Ni kweli, Kanye West ni rapper mmoja tu hivi wa Marekani, anayependa fashion na aliyebahatika kumuoa mmoja wa wanawake wenye nguvu katika burudani duniani, Kim Kardashian. Na pia wakati mwingine hufanya vituko vingi vinachowaacha mdomo wazi watu wengi. Lakini nyota huyu ana harakati anazozifanya ambazo zinaweza kuwa na funzo kwa mjasiriamali wa Tanzania.
Haya ni mambo matatu muhimu mjasiriamali wa Tanzania, hasa mchanga anaweza kujifunza kutoka kwa Yeezy:
1. Ifanye familia yako washingialiaji wako wakuu
Kwa maisha ya Kitanzania, si watu wote ambao huungwa mkono na ndugu ama jamaa katika miradi wanayoifanya. Wakati mwingi wajasiriamali huamua kufanya wanachokipenda bila kupewa baraka zozote na watu wa familia yao. Kwa Kanye lakini, amebahatika, ama wakati mwingine amewalazimisha watu wake wa karibu hususan ndugu wa ukweni kwa Kardashian na marafiki zake kuwa naye bega kwa bega katika miradi yake.
Kanye anapenda fashion na amehangaika kwa miaka sasa kutengeneza himaya yake ambayo walau sasa imeanza kumlipa vyema. Nguo zake za Yeezy, Pablo na chapa zingine, zimeanza kumuingiza fedha nyingi. Kwa kuongeza na mauzo ya muziki wake, mwaka huu Kanye ameingiza dola milioni 17.5, kwa mujibu wa Forbes. Mke wake, Kim Kardashian ni mshangiliaji mkuu wa kazi zake na amekuwa bega kwa bega na mume wake kwenye harakati hizo.
381344c900000578-0-image-a-1_1473375656385 Kim akiwa amevaa nguo za Pablo zinazotengenezwa na mumewe, Kanye West
Kwa mjasiriamali wa Tanzania, ni vyema akatambua kuwa support ya watu wa karibu katika mradi wake ni muhimu sana. Hao ndio watu watakaokupa moyo na ari ya kuendelea kupambana kuifikia ndoto yako pale unapokata tamaa. Kwa wale waliobahatika kuwa na support hiyo, watambue kuwa wana bahati na waienzi.
2. Amini wazo lako, usiyumbishwe na wanaokukatisha tamaa
Kuna wakati watu humuona Kanye kama mwendawazimu hivi. Amekuwa na ndoto za mwezini, lakini hajabadilishwa na maneno ya kukatishwa tamaa. Miaka miwili iliyopita, alikuwa na msongo mkubwa wa mawazo kutokana na ugumu aliokumbana nao kutimiza ndoto zake katika ulimwengu mpana mitindo.
Mwanzoni mwa mwaka huu alidai kuwa amewekeza takriban dola milioni 53 katika fashion ambazo bado hazijarudi. Aliwashangaza zaidi watu pale alipomtaka CEO wa Facebook, Mark Zuckerberg, awekeze dola bilioni 1 kwenye ndoto zake. Huyo ni Kanye, licha ya kupuuzwa, Yeezy aliendelea na harakati zake na sasa anaingiza mkwanja mrefu.
Hivi karibuni alifungua maduka ya muda katika majiji 21 duniani kuuza nguo zake za Pablo. Katika duka la New York pekee alidai kuingiza dola milioni 1 kwa siku mbili tu.
complex-kanye-west-life-of-pablo_ah_01_o49686 Msululu mkubwa wa wateja waliokuwa wakitaka kununua nguo za Kanye West
Kama mjasiriamali, kuamini katika ndoto yako ni jambo la msingi sana. wewe ndiye unayejua kwanini umeamua kufanya biashara ya matikiti maji, hukuambiwa na mtu. Katika duniani hii, utakutana na maneno mengi ya kukukatisha tamaa na kubeza unachojaribu kufanya. Amini katika wazo lako, kwakuwa unajua unachokifanya, utafanikiwa.
3. Kuwa Wewe
Kuna mawazo mengi sana ya kufanya, kwanini uamue kufanya kile kile kila mtu anafanya? Kwanini wote tupite njia moja? Katika ulimwengu wa fashion, Kanye alipigwa vita sana mwanzoni wakati anazindua nguo zake za Yeezy! Wengi walibeza kuwa ni nguo za ajabu ajabu zinazoonekana kama za watu watu fukara.
kanye-west-yeezy-season-2-0
Kwakuwa Kanye, hakutaka kufanya kile wabunifu wengi hufanya, aliamua kuzipa upekee nguo zake. Licha ya kubezwa, nguo hizo zimekuwa zikinunuliwa kwa kiasi kikubwa na akaunti zake za benki zimeendelea kucheka tu.
Kuna tatizo kubwa la kuigana kwa biashara hapa Tanzania. Kila mtu anataka kuwa na kibanda cha M-Pesa, kila mtu anataka kuwa na Bajaj au Bodaboda na biashara zingine maarufu nchini. Ni muda wa kufikiria nje ya boksi na kuwa na mradi wa pekee utakaokuweka kwenye njia yako mwenyewe. Si vibaya kufikiria kwa mtazamo wa Kanye!

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM