Tuesday, 13 September 2016

Hivi Ndivyo Muziki wa Singeli ulivyogeuka dhahabu ndani ya kipindi kifupi

Nilianza kuusikia muziki wa Singeli mwaka na nusu uliopita na zaidi kwenye Bajaj nilizokuwa napanda. Sikuuelewa kabisa muziki huu na mara nyingi niliona ukinipigia kelele tu.
singeli
Nilikuwa najiuliza ni kipi hasa watu hawa walikuwa wanaimba na tena wakiwa na mfumo na njia zao wenyewe. Ni kama vile walipita shule moja na kujifunza uimbaji wake. Ama hakika muziki huu ulikuwa ukinishangaza sana. Kwa wengi pia muziki huu ulionekana wa vijana wahuni wanaoishi maeneo ya uswahilini. Lakini watu wanaojua, wanasema umekuwepo mtaani kwa zaidi ya miaka 10 sasa na ulikuwa maarufu kwenye sherehe za uswazi kama vile vigodoro na zingine.
Ni muziki ambao wakati mwingi ulikuwa ukiimbwa na wahuni, vibaka, wavuta bangi na wengine mateja. Kwa mujibu wa Kicheko, mtu muhimu kwenye muziki huo, Singeli ni muziki uliokuwa ukiimba na vijana waliokuwa na stress na ulitumika kama njia ya kuzipunguza.
Miaka mitatu iliyopita, hakuna kituo cha redio kilichokuwa kinautambua muziki huu kama wenye kiwango na ubora wa kuchezwa hewani. Japokuwa kulikuwa na muziki wa uswazi kama mnanda wa wasanii kama Omari Omari uliopenya mainstream, muziki wa Singeli ulianza kuchezwa zaidi miaka miwili iliyopita.
Na hakuna anayeweza kubisha kuwa EFM wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye ukuaji na kisha kukubalika kwa Singeli. Wao walitenga kabisa vipindi vya kucheza muziki huo kikiwemo Genge. Lakini pia EFM ilikuwa ikicheza muziki huo hata kwenye vipindi vya asubuhi (Breakfast show), kitu ambacho hakuna redio iliyokuwa ikifanya hivyo.
“Heri ya kuzaliwa kaka mkubwa !! @majizzo naweza kusema wewe kwa binafsi yako una mchango mkubwa kwenye mziki wetu wa #singeli,” aliandika nyota wa Singeli Sholo Mwamba alipokuwa akimpongeza CEO wa EFM, Majay kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Katika kipindi hiki kifupi muziki wa Singeli umezalisha mastaa wakiwemo Sholo Mwamba na aliyekuwa Dj wake, Man Fongo. Lakini pia wasanii wa Bongo Flava kama Rama Dee na Profesa Jay wametoa nyimbo zao wakiwashirikisha waimbaji wa Singeli, Young Yuda na Sholo Mwamba. 

 Sholo amefahamika kwa wengi kupitia wimbo ‘Kazi’ wa Profesa Jay, huku Man Fongo akipenya kwa wimbo wake ‘Hainaga Ushemeji’ na kumtumia Shilole kwenye video yake. 

Haikuchukua muda hadi makampuni ya simu yakiwemo Tigo na Vodacom yaliyotengeneza matangazo kwa muziki wa Singeli. Muziki huu una nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri hasa kwakuwa umeendelea kujikusanyia mashabiki wengi. Kikubwa, ni muziki wenye asilimia 100 ya ladha za Kitanzania, na kuufanya siku za usoni uwe na thamani kubwa nje.
WANAMUZIKI WA BONGO FLAVA WANAUNGUMZIAJE?

“Sisi watanzania tumekuwa na muziki ambao haueleweki, hata hip hop tunayoifanya inayoweza kumuonesha huyu ni mtanzania ni Kiswahili tu,” alisema Profesa Jay kwenye mahojiano kuhusu muziki huo.
“Nimefanya hip hop singeli kwaajili ya kuupeleka muziki huo mbali lakini pia kuitengeneza hip hop tofauti. Kuliko kuwakopi akina Lil Wayne wanafanyaje basi tufanye muziki ambao tutakopi muziki wa nyumbani. Nadhani ni muda sasa hivi wasanii wa hip hop kutanua, wasikopi vya Marekani, wako vya Tanzania ili kuifanya hip hop yetu ibadilike kila siku,” aliongeza.
Kwa upande wake Rama Dee pia alidai kuwa marafiki zake wa nje waliushangaa wimbo wake ‘Mazoea’ wenye ladha ya Singeli na RnB na kudai kuwa ni muziki wa tofauti. “Naupenda, ni muziki mzuri sana. Walishangaa sana kwamba nawezaje kufanya vile kwasababu mimi nasound tofauti kidogo halafu muziki unasound Kiafrika kwahiyo nimechanganya kiasi kwamba mpaka sound imetoka nzuri sana, kwahiyo wanapenda sana,” alisema.
Vanessa pia anautabiria makubwa muziki huo.
“The drum percussion is so unique,” alikiambia kipindi cha 5 Select cha EATV mwezi uliopita. Aliongeza kuwa maproducer wakubwa kama Major Lazer na Pharrell Williams wamekuwa wakiufuatilia muziki wa Afrika kwa ukaribu na huenda masikio yao yakaja kutua kwenye muziki wa Singeli.
VITA VYA MAFAHARI KATIKA REDIO: EFM VS CLOUDS FM
Kwa sasa si EFM pekee inayocheza muziki huo kwa kiwango kikubwa. Miezi ya hivi karibuni, Clouds FM nayo imeonesha kuupokea muziki huo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu imewapandisha kwenye jukwaa la Fiesta wasanii wa Singeli akiwemo Man Fongo ambaye amedhihirisha kuwa si muziki wa Dar pia, bali umekubalika Tanzania.
Clouds imeenda mbali zaidi kwa kuwaumiza kwa mara nyingine EFM kwa kumchukua mtangazaji wa kipindi chao cha muziki huo, Genge, Kicheko. Mchekeshaji huyo mwenye historia kubwa na muziki huo hadi kuwa na label yake ya ‘uswazi’ yenye wasanii kibao akiwemo Ferooz, amejiunga na Clouds FM ambako ataanzisha kipindi kiitwacho Flava za Uswazi.
14269048_324682454544384_415668090_n Kicheko aka Rais wa Uswazi akikaribishwa Clouds FM Jumanne hii kwa shangwe kubwa
Kicheko amekaribishwa kwa shangwe kubwa Jumanne hii na kutambulishwa rasmi kupitia kipindi cha Leo Tena kilichorushwa pia live Clouds TV. Pamoja na kuchukuliwa mtangazaji wao, EFM haioneshi dalili za kuacha kuupa kipaumbele muziki huo kwakuwa kupitia kampeni yake ya Muziki Mnene: Tunasepa na Kijiji wameendelea kutafuta vipaji vya Singeli.
MUZIKI WA SINGELI NI WA KUPITA?
Si mara ya kwanza kwa muziki mgeni kupanda chati na kupendwa na watu. Lakini historia inaonesha kuwa, kuna muziki uliowahi kutamba lakini haukudumu. Kwa upande wa Singeli, naamini hautakaa milele, lakini utakaa kwa muda mrefu. Ni kwasababu muziki huo umekishika hadi kizazi cha watoto wenye umri mdogo wanaonekana kuupenda na kuuimba.
Hiyo ina maana kuwa kuna kizazi kingine kinatengenezwa kitakachouwakilisha muziki huo kwa muda mrefu. Kwa jinsi ambavyo vituo vya redio na TV vimeonesha kuukubali, nyota wengi wakubwa wa muziki huo watazaliwa na utageuka kuwa ajira kubwa kwa vijana, kama tu jinsi Bongo Flava ilivyofanya.
Sababu nyingine kubwa ni kuwa waimbaji mastaa wa Singeli wamejichanganya na waimbaji wa Bongo Flava na pia hata video za muziki wao zimekuwa na ubora mzuri kama tu nyimbo za wasanii wengine. Ni wasanii ambao wanauchukulia serious muziki wao.
Mtu mwingine muhimu wa kumkumbuka kwenye ustawi wa Singeli ni producer Mesen Selekta. Huyu ndiye producer wa Bongo Flava aliyengeneza hits nyingi zaidi za Singeli zikiwemo ‘Hainaga Ushemeji’ ya Man Fongo na Singeli ya Sholo Mwamba na ‘Kazi ya Profesa J aliyomshirikisha Sholo.

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM