Friday, 19 August 2016

NI KWELI KUZOEANA SANAAAA....KUNAPUNGUZA MAPENZI?


Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa kabisa na unaendelea na majukumu yako ya kila siku!. Leo ningependa tujadiliane kuhusu hiki kinachosemwa na wengi kwamba mkishakaa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu, mnazoeana na mkishazoeana mapenzi yanapungua kati yenu na mwishowe mnaanza kuishi maisha yasiyo na msisimko wa kimapenzi. Leo sitaki kuwa mzungumzaji mkuu kwa sababu naamini wengi wetu tumewahi kuishi kwenye uhusiano wa kudumu na wengine bado tupo kwenye uhusiano wa kudumu hadi leo, iwe ni ndoa, uchumba au mapenzi ya dhati ambapo mwanaume na mwanamke wanaishi pamoja. Kwa upande wako, hebu jiulize, mmezoeana kiasi gani na mpenzi wako? Kipindi ambacho ndiyo mlikuwa mnayaanza mapenzi, bila shaka hamkuwa mmezoeana, je, ukilinganisha mapenzi ya kipindi hicho na sasa baada ya kukaa na mwenzi wako kwa kipindi 
kirefu, wapi penzi lenu lilikuwa na msisimko? Bila shaka kila mmoja atakuwa na majibu yake, ninachotaka hapa ni kujadiliana ili mwisho tufikie muafaka kwa lengo la kuboresha uhusiano na wenzi wetu. Binafsi nalitazama suala la kuzoeana sana na mwenzi wako katika sura mbili tofauti; sura ya kwanza ni yale mazoea mazuri, ambayo unazoeana na mpenzi wako kiasi cha kumchukulia kama rafiki yako kipenzi, kwamba mambo yako yote unamwambia, hata zile siri ambazo huwezi kumwambia mtu mwingine yeyote na yeye za kwake 
anakwambia. Sidhani kama kuna tatizo lolote kuzoeana na mwenzi wako kwa kiwango hiki. Wengine huenda mbali na kufikia hatua ya kuvaliana nguo au ‘kushea’ vitu mbalimbali, mnapofikia hatua hii mnakuwa mmeshibana sana! Mkikaa pamoja lazima mtataniana, mtachekeshana, mtafurahi na moyo wa kila mmoja utakuwa na furaha kubwa kwa mwenzake. Mkiwa mmeshibana namna hii, hata mwenzi wako akienda kazini, utaona kama saa haziendi haraka, utatamani arudi haraka au kama wewe ndiyo upo kazini, utatamani muda wa kutoka ufike haraka ili ukakutane na kipenzi chako, rafiki yako na msiri wako. Umeshawahi kuishi maisha ya namna hii? Kama bado basi jihesabu kama bado hujayafaidi mapenzi! Amini nakwambia, mkiwa mnaishi kwa mtindo huu, akili zako, moyo wako na hisia zako zote utazielekeza kwa mwenzi wako, utampenda na kumfanyia mambo mazuri mpaka watu wanaowazunguka watakuwa wanawaonea wivu... mtakuwa mnaishi kwenye penzi hai, lenye msisimko na bashasha za kila aina.


 Hata hivyo, huo ni upande wa kwanza wa mazoea! Upande wa pili ndiyo ule ambao huwa unawatoa machozi wengi; mazoea mabaya. Wakati mnaanzisha uhusiano wenu, mwenzi wako alikuwa akikuheshimu sana, ukimwambia jambo mara moja tu ameshatekeleza, ukimuomba kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wake, yupo tayari ajinyime lakini akupe. Hata kama alikuwa na marafiki zake au ndugu zake, akikuona yupo tayari aache kila kitu na kuja kwako, atakusikiliza, atakunyenyekea na kukupa heshima ile unayostahili. Hata hivyo, kadiri mtakavyokuwa mnazidi kukaa pamoja na kuzoeana, utaanza kuona mabadiliko. Ukimwambia jambo ni lazima urudie hata mara tatu ili akuelewe, utamueleza kwa nia njema kwamba jambo fulani sipendi ulifanye lakini mkishamaliza kuzungumza tu, yote anayaacha hapohapo! Anachukulia kwamba amekuzoea kwa hiyo huwezi kumfanya chochote, matokeo yake atafanya tena kile ulichomkataza, tena kwa makusudi. Alikuwa na kawaida ya kuwahi kurudi nyumbani lakini kwa kuwa mmezoeana, yuko radhi akakae na marafiki zake mpaka usiku, bila hata kutoa taarifa akiamini huna cha kumfanya. Hakuoneshi heshima tena, kila kitu anachukulia rahisi tu, haoni vibaya kukuita majina mabaya, kukupa sifa mbaya na kukudhalilisha kwa sababu tu mmezoeana, anajua huna cha kumfanya! Hata kupeana haki ya ndoa linakuwa siyo jambo la muhimu tena na hata akikupa inakuwa ilimradi liende! Kisa, mmezoeana na hakuna tena kipya kati yenu. Haya ndiyo mazoea yanayotajwa kuchangia sana kupunguza au kuua kabisa mapenzi. Kwa upande wako hali ikoje? Tuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa namba za hapo juu. Tukutane wiki ijayo.
 
 http://www.bongohotz.com

No comments:

Post a Comment

FIND US ON FACEBOOK

Followers

FOLLOW ME ON INSTAGRAM